BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX
Photobucket

Tuesday, May 18, 2010

NGOMA MPYA YA TIZZLE- KUTOKA TANGA MPAKA LONDON!!

(Tizzle na Damuz)

Msanii kutokea jijini Tanga anayejulikana kwa jina la Tizzle ambaye hivi sasa anaishi nchini Uingereza kuonako jiji la London, amechia ngoma yake mpya inayoitwa 'Nameless' aliyomshirikisha Damuz.

Akiongea na Blog hii moja kwa moja kutokea Uingereza, Tizzle amesema kuwa ngoma hiyo ameifanya pale studio za East London kwenye studio moja inaitwa Mzuka Entertainment Rec chini ya producer Josh.

Tizzle aliongeza kuwa, anaamini ngoma hiyo itamuweka pazuri kunako ramani ya Bongo Flava na duniani kwa ujumla kwa kuwa ina kiwango cha kimataifa. Sikiliza wimbo huo hapo juu palipoandikwa SIKILIZA TANGA FLAVA HAPA! Song: NamelesS, Artist: Tizzle feat Damuz

Msanii huyo ambaye kabla ya kwenda Uingereza alikuwa anaishi pale Majani Mapana na baadae kuhamia Bara Bara ya 15, kwa sasa yupo anajipanga kutoka na ngoma nyingine ya 'Hisia Zangu' ambayo atawashirikisha washkaji zake damuz, josh pamoja na danny.

Mpango wa albamu unakuja na ataipa jina punde tu itakapokamilika.



MITAA YA TANGA CITY LEO ASUBUHI!!!







Monday, May 17, 2010

TUJIKUMBESHE NA 'MBADO' YA MR EBBO

'LYRICS YA MR PRESIDENT'- NGOMA YA ROMA


SONG MR-PRESIDENT
ARTIST R.O.M.A
PRODUCER J-RIDER + YUDDI
STUDIO TONGWE RECORDS
romabraq@yahoo.com


INTRO
By…..Mwl. Julius Kambarage Nyerere
Ikulu ni mahali patakatifu, ikulu ni mahala patakatifu,
Mimi sikucha guliwa na wananchi wa Tanzania
Kuja kupageuza kuwa pango la walanguzi
Claps claps claps
By…Roma
Drop drop drop drop drop yop
Haaa haaa… yes Surprise …Tongwe records
We are here for revolution wooord
Mr. president ..welcome to white house
Thank you….aaaah …thank you ….yeaaah

VERSE….1
Mi ndo’ roma mkatoliki mwenye asili ya kiyahudi
Mpare wa milimani sa lamu ya kikwetu urewedi
We ni mkwere wa chalinze ambaye hutamsahau mnyakyusa...(Mwakyembeee)
Aliye wafundisha monduli siasa
Aliyekula kiapo kwa agano jipya la wakorintho
Siyo msabato mwenye siasa za kubattle kama Zitto
Mwenye wito wa Appocalypto husssle za Kambikatoto
Msaka ndoto kama kristo shujaa kama Mrisho Mpoto
Jasiri kama Mandela busara kama Nyerere
Niliyejificha mapangoni mithili ya Otango Osale
So usinidanganye kwa uchawi waaa kutumia ndulele
Au vita vya majimaji nife kama Kinjekitile
Hatutaki siasa za kale, siku hizi tunawahi kubalehe
Nawapa pole wakazi wote wa Tandale kwa Mtogole
Akhsante Sheikh umeniita ikulu sio kisa nina nyota ya mshale
Najua mvi sio busara ila naomba amani itawale
Ikulu yako ina thamani zaidi ya falme za kiarabu
Cha ajabu hawaithamini na inapoteza thawabu
Taifa lilikutabri tangu enzi ukiwa waziri
J.K wa 2 utakuja ongoza hii serikali
Yenye vilio kote kama kina mama wa Galilaya
Wanaoutafuta ukombozi wasimamishe Pobilahaya
Viongozi wetu ni mafia na mabeautifull lier
Nilikuwa na ndoto hizo ila bado hawaja niinspire

CHORUS
Pagani si mlituahidi mtamwaga na lami vipiii?...Badoooo
Wanafuzi mlituahidi walimu mtawaleta!!...woooh
Morogoro na Tanga vipiii?Badooo
Dodoma…?Badooo…
Kigoma…?Badooo..
Maisha bora kwa watanzania nyie wenyewe mlituambia
Manurse…?Badooo
Mapolice…?Badooo
Ajira kwa vijana na maendeleo kwa kina mama
Watotoo…?Badooo
Kina mamaaa…?Badoooo

VERSE….2

Inafahamika ulipewa nchi angali imeshachafuka
Uongoze hii familia kubwa ya kizazi cha nyoka
Na ukakubali kubeba huu msalaba wa ukombozi
Hizi kashfa ndo’ changamoto zisikutoe machozi
Sitosahau campaign zako za mwaka 2005
Nilichomwa na jua nikingoja upite nipunge mkono
Traffic aliyepangwa saa moja kisha ukapita saa saba
Akiwa na stress za mwanae shuleni kafukuzwa ada
Leo mna nyumba mna mashamba mna viwanja mna viwanda
Mi nasaga na rhumba na mshahara wangu haujapanda
Yule traffic maisha magumu aaah muogopeni Mungu
Nikisema it is not fair mnataka mnifunge pingu
Gerezani kesi za wanyonge cheki zinapigwa tarehe
Jamhuri itafata mkondo ee mola wangu wasamehe
Wasaliti kama Eskarioti mbele ya Yesu Mnazarethi
Wa sakramenti ya ekaristi bado hawaitaki torati!!
Harakati ndo’ jadi siogopi hadi wanichape mjeledi
Hadi yuddi alikuwa shahidi kwa vinanda na vinubi
Elimu yetu bahati nasibu kama mikopo ya desi
Kimbilio la waliofeli ni ualimu na upolisi
Wamefisadi tenda ya rada, ndege ya raisi, magari ya jeshi
Wote matraitor sasa skrepa kama Lubumbashi
Wanapata alama za juu kwa kumuhonga penzi professor
Mtunza pesa wa benki kuu kumbe pepa zote alidesa
Au unataka 2010 mapinduzi yawe ya Liberia
Eti utajiri ni mbuga, milima na ziwa Vicktoria
Piga vita ujinga, umasikini na H.I.V carriers
Askofu kutawala nchi hatutaki hizo elimu dunia
Migomo ya chuo kikuu naitupia jicho la 3
Sitetei mpaka Rutashoborwa akiwa wakili kisutu
Kul - nafs - dhal - kal - maut inasema torati
Rest in peace shusha bendera ipepee nusu mlingoti
Bungeni hawaijadili bajeti ya mlala hoi
Mtu hataishi kwa mkate bali neno siyo divai
Tazama timu yako iliyoko madarakani
Na mchunguze kwa makini anayelia sana msibani.

CHORUS

Walimu si mlituahidi mtatupa hela zetu vipiii…?Badooo
Mitihani si mliahidi haitavuja tena….woooooh
Nachingwea na Mbeya vipiii…?Badooo
Tabora…?Badooo
Mtwara…?Badooo
Maisha bora kwa watanzania nyie wenyewe mlituambia
Wamachinga…?Badoooo
Wakulima…?Badooo
Ajira kwa vijana na maendeleo kwa kina mama
Wazee…?Badooo
Vyuo vikuu…?Badooo

VERSE….3

Huu sio wakati wa kuwaua maalbino
Angalau mapinduzi kama Macio Maximo
Usihangaike kumtafuta Roma…mi!! Hakimu wa getho
Mwenye sauti ya mamlaka!!! iliyomfikisha Mrombo Keko
Baada ya kukemea ufisadi na sera za Karamagi
Na waliokula jasho letu kwenye migodi ya Buzwagi
Utazuia vipi ongezeko la wimbi la ukeketaji…
Wakati Ngariba ndo’ diwani wa kata kwenye kijiji!!
Neither do I…!! hongera ulipima ukimwi
Watanzania nasi tuamke tusimpige kibao tu Mwinyi
Hapa nagundua aya-tul - munafik - thalatha
Inawezekana aliishia alifu wakati anasoma madrasa
Huu sio muda wa kujadili kesi za Manji na Mengi
Hayo ya Mungu we Kaisari jadili mambo ya msingi
Teacher alipojiita mtabiri Tanganyika wote vipofu
Padre wa kwanza pentekoste ubatizo wa maji marefu
Machozi yalinitoka Segera watoto hawapati haki
Wengi wamekimbia shule basi lije wauze visheti
Wanaosomeshwa kwa mtaji wa chapati na uvuvi wa samaki
Wabunge wao wamekaa na wanajiita wanaharakati!!
Rudi kwenu kahamasishe nduguzo hawana taaluma
Wazaramo wamegoma soma still mwali wanamcheza ngoma
Wanalia Kilwa Kivinje huku wanaocheka ni wabunge
Walionunua kura ya bibi kwa kumuhonga doti ya kitenge
Hata wamasai walikuchagua kwa kura nyingi za upendo
Wakiamini mtetezi yuaja wa jimbo la Oldoyo Sambo
Waambie what is going on ndani ya himaya ya bwawa la Mtera
Waonyeshe na mikataba ya utawala wa mgodi wa Kiwira
Jeshi lote kwenda Tarime hawakuwa na njia mbadala
Na walioteketea Mbagala!!
Mr.pres …. Haya masikharaaaa!!!
Sina maana utoke wewe hicho kiti umuachie professor
Nisamehe kama nakosea maana mimi sio mwanasiasa
Claps claps claps

OUTRO
By…Mwl...Julius Kambarage Nyerere
Kwa hiyo kitu kimoja tunataka kuelewa…
ni hali ya matatizo ya nchi yetu yalivyo sasa hivi....Eee!!
Kwasababu...sera ya...ay..…awamu ya kwanza…. awamu yangu mimi…
imefanya mema…. imefanya ya kijinga….
ya kijinga yanaachwa…!! lazima yaachwe….
Ubaya wenu ni kwamba…. mnaacha mema...mnachukua ya kijinga.

MISS PANGANI SASA NI TAREHE 29/05/2010


Kutokana na maboresho yaliyojitokeza, Miss Pangani sasa imesogezwa mbele hadi tarahe 29/05/2010 badala ya ya tarehe 21/ kama ilivyokuwa imepangwa ili kukidhi haja za mashabiki wake. Tunaomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza. Dont Miss It...!!!

TANGA YANG'AA TUZO ZA KILI!! MISOSI, CP WAIBUKA KIDEDEA

Msanii Bwana Misosi kutokea jijini Tanga akishangilia tuzo ya wimbo bora wa Ragga aliyopewa na Sean Kingston.

Hasheem Thabeet akimkabidhi msanii kutokea Tanga City CP tuzo yake ya video bora ya muziki ya mwaka kupitia wimbo wake wa Problem.

Friday, May 14, 2010

ASILI, MILA NA DESTURI ZA KABILA LA WAZIGUA!!

Lugha yao ni Kizigula.

ASILI, MILA NA DESTURI ZA KABILA LA WAZIGUA. Wazigua ni mojawapo wa makabila ya asili ya mkoa wa Tanga. Wazigua ambao lugha yao ni ya jamii ya lugha za kibantu yasemekana wamekuwepo mkoani Tanga, wilaya ya Handeni kwa karne nyingi zilizopita.

Maana ya ZIGUA ni kuchukua au ukamata eneo. Miaka mingi iliyopita Wazigua walipigana vita na kuyashinda makabila ya Wabondei na Wasambaa. Makabila hayo yaliyoshindwa vita yalikimbiliia maeneo ya mabondeni na mengine kusambaa milimani, Wabondei huko Mabondeni, na Wasambaa walisambalia milima ya USAMBARA. Na ndio chanzo cha majina ya makabila haya, kwani kabla ya hapo walikuwa wakiishi pamoja kama koo za jamii moja. Na walijulikana kwa jina la BOSHAZI maana yake Bondei, Zigua, Sambaa.

KUMTAMBUA m-BOSHAZI Unaweza kumtambua m-boshazi kwa jina lake kwa mfano mzigua Samamboe, Sakuzindwa, Sannenkondo, Sankanakono, Shundi, Butu, Chamdoma nk. Kuzungumza kwao huvuta maneno, mfano wa kusalimiana, Ahooni niheedi hanginyuwe, nk.

Msambaa utamtambua kwa jina lake, mfano Shekimweli, Sherukindo, Shekiondo Shekazi, Shemndorwa, nk. Hawa wote ni wasambaa na hutamka maneno yao ulimini, mfano, tinakwenda, titarudi, titaonana kesho, nk.

Wilaya ya Handeni pia kuna makabila mbalimbali kama Wakilindi, Wanguu, na Wasambaa..


Katika Karne hii ya sayansi na tekinolojia, na kutokana na utandawazi, makabila mengi ya kiafrika yamekubwa na mabadiliko yasioepukika katika mila na desturi zao.

Mila ya kutahiri wanawake imekuwa ikipigwa marufuku na serikali mbalimbali za ulimwenguni kuwa ni kinyume cha haki za binaadamu, hivyo basi kuna mila ambazo zinakomeshwa na serikali za nchi na nyingine zinapotea zenyewe taratibu kutokana na kubadilika kwa hali ya maisha, hivyo ili kutunza mambo haya yasije kusahaulika vyema kuweka kumbukumbu ya asili zetu. Tumetumbukia katika masuala ya utandawazi kiasi ambacho tunashindwa hata kutambua miiko yetu au asili zetu, kwa kweli ni mambo ya kusikitisha sana si ajabu kwetu sisi wazee tutakapoondoka basi haya nayo yatapotea.

Katika kabila la Wazigua, kutoa majina kwa watoto wanaozaliwa huzingatia wakati, mahali, na mahusiano. Kila mzigua lazima awe na jina la asili na la kidini, mfano Andrew Kizenga Shundi jina lake la asili anaitwa Chamdoma (dyauta netangwa Chamdoma, Dyamwale), kiasili majina hutolewa wakati mtu anapozaliwa(Chamdoma), Dyamwale anapotoka kutahiriwa na kuchezewa ngoma na kukabidhiwa upinde, na hivyo hupewa jina na kuwa kijana wa kizigua aliyefikia utu uzima. Anapooa huitwa Samachau, na anaeolewa Wanamachau.

Kwa maana hiyo baada ya kumaliza tukio la kuoa na kumaliza deni la mahali na vihendo (zawadi au vitu vitolewavyo kutoka upande wa muoaji kwenda kwenye familia ya muolewaji) ulivyotakiwa kupeleka ukweni kwa mfano zawadi kama zogoro dya chunji, koti dya sachibwela, ngubula mlomo, kisingisa magutwi, kumwonelahi, Nk.

Basi hayo mambo ya asili ya kizigua, ambayo kabila hili hujivunia. Wazee wa kizigua kama Marehemu Mzee Gerald Fredrik Kizenga Shundi ambaye ni mzaliwa wa Handeni (Mandela), alikuwa mtoto wa kwanza wa mzee Fedrik Kizenga Shundi na ni mmoja kati ya watoto 8 wa Mzee huyu alizaliwa na mama TEREZA, huyu bibi asili yake ilikuwa Vugiri huko Kwa magome. Mzee huyu (Gerald) alikuwa akihimiza vijana kwa wazee kudumisha mila na desturi za kizigua katika uhai wake.

Kwahiyo miji ya asili ya Wazigua wa ukoo wa Shundi na chimbuko la Mzee Gerald Shundi ni Mandela ya Handeni na alikuwa ni wa MWEMNUN’GULI SAMNANDUGWA upande wa Baba yake, ni Chiva na Nunguli ni upande wa mama mwanae Andrew Kizenga Shundi, asili yake ni Pongwe ya KIDELEKO kama unakwenda Kwa Magome.

Mila na desturi za Kizigua kama zilivyo mila nyingine za kiafrika zina miiko yake kwa mfano, “HACHIKUNGIGWA KUDYA MBARA UNADYA AU UNAGONELA UMKOTA WA MBARA WABAMBUKA/ WAHOLOMOKA MWILI MJIMA” Maana yake Mzigua hatakiwi kula Paa (mnyama).

“KULAGASAMA” ni tukio la kuagwa kwa waliooana mara baada ya kukamilisha mahari na taratibu zote za kimila. Katika mila za Kizigua, mtu anapofunga ndoa, yeye na mkewe hutakiwa kukaa katika familia ya mke wake huyo kwa muda fulani ili aweze kukamilisha mahari kama alikuwa hajamaliza. Hivyo kumaliza kulipa mahari na mambo mengine yanayohitajika, huomba ruhusa toka kwa wakwe zake ili akaanzishe maisha yake na mkewe.

Na kama akishindwa kulipa ataendelea kuishi upande wa mkewe kwa maisha yake yote na hata kama akifariki atazikwa upande wa ukweni kama ukoo wa upande wa mume hautamlipia, kama wakimlipia watapewa mwili kuzika upande wa mume.

Wazigua wana ngoma nyingi za asili na huchezwa kutokana na wakati na tukio husika, mfano kuna ngoma za wakati mavuno, harusi, jando na msibani, hujulikana kwa majina ya Mkweso ,Machindi , Tukulanga, nk.

Pia mtoto akishazaliwa hukaa ndani na baada ya siku 40 hutolewa nje na kupewa jila la Lungo. Katika tukio hili la kumtoa mtoto nje, mtoto hupakwa unga na kunyolewa nywele zake za utotoni na bibi yake na mtoto ambaye mara nyingi huwa ni mama wa baba yake na mtoto.

Vyakula vya asili vinavyopendelewa kuliwa na wazigua ni ugali unaopikwa kutokana na unga wa mahindi yaliyokobolewa na kuvundikwa kwa muda mrefu kabla ya kusagwa au kutwangwa. Baada ya kysagwa hutoa unga mweupe na laini sana. Ugali huliwa na mboga za asili kama vile, Kungujulu, Sunga, Kididi, Mnavu, nyama za pori na uyoga.

Maneno ya kizigua na maana zake kwa Kiswahili. Kizigua Kiswahili Mgosi Mwanaume Mwana Mtoto Mwana wa Chigosi Mtoto wa Kiume Mwana wa Chivyele Mtoto wa kike Uta Upinde Nguku Kuku Biga Mtungi Mazi Maji Uchi Asali Sila Barabara

UNAIJUA VITA YA TANGA.!!? ISOME HAPA

Thursday, May 13, 2010

'VISA NA MIKASA NDANI YA TIP TOP'- TALE

Akiwa kiongozi wa kundi la Tip Top Connection kwa muda wa miaka 12, tangu alipoanza kuunda kundi hilo mwaka 1998 akiwa na Madee, Babu Tale amevunja ukimya na kuamua kuelezea visa na mikasa alivyokutana navyo akiwa kama kiongozi wa kundi hilo.

Hili lilitokana na tetesi zilizoenea kwamba kiongozi huyo ana mpango wa kumrudisha Mb Dog ndani ya kundi hilo soon, hivyo nilimtafuta kiongozi huyo ili aweze kuelezea mkakati wake.

Khamis Shabani Taletale a.k.a Babu Tale anaanza kwa kusema nieleza kwamba taarifa hizo ni za kweli na hivi sasa yupo katika maandalizi ya kumrudisha msanii huyo ikiwa atakuwa tayari kuungana na kundi hilo tena kwa mara ya pili.

Hata hivyo Tale alipoulizwa kuhusiana na maamuzi ya wasanii wengi kuchomoka ndani ya kundi hilo na kila mmoja kuelezea sababu iliyomfanya atoke, licha ya sababu zao kufanana lakini Babu Tale alieleza kuwa sababu hizo si za msingi.

Mb Dog, alitangaza kudhulumiwa
"Sina ubaya wala matatizo na Mb Dog kwani aliondoka ndani ya kundi bila kukwaruzana, lakini kilichonisikitisha nilimsikia katika mahojiano na vyombo vya habari akielezea kuwa uongozi wa kundi ulikuwa haumtendei haki.

Tale alielezea kuwa kurudi kwa Mb Dog kutakuwa na mabadiliko ambayo yatakuwapo ndani ya kundi na itategemea namna msanii mwenyewe atakavyokubaliana na uongozi wa kundi.

Hata hivyo alieleza kuwa kuna wasanii wengi sana ambao hivi sasa wanatumia mgongo wa Mb Dog bila mwenyewe kujua, hivyo iwapo atasimama chini ya mwamba imara ataweza kurudi upya na kwa kasi kubwa kwenye game.

Spark, 'Nipe ripoti' ya Tundaman
"Msanii huyu alikuja kwangu mikono nyuma lakini siamini katika kile ambacho amenifanyia katika kipindi cha mwisho, mimi sio Mungu lakini sidhani kama nitampokea tena ndani ya kundi langu.

"Nilimsaidia kwa kiasi kikubwa sana mpaka alipoweza kufika alipofika, lakini baadaye alianza kuwa na utovu wa nidhamu hali iliyosababisha tumkanye mara kwa mara nikiwa na Abdi Bonge (mwekezaji katika kundi) lakini haikusaidia.

Tale anasema, kutokana na tatizo la Spark kutokupata shoo baada ya kutoa singo yake 'Usiniache' Bonge alishauri watoe albamu ya pamoja na Tundaman ili waweze kunyanyuana.


Z' Anto, nilimkuza kisanii nashangaa alinikashfu
"Kwa madai yake alisema kwamba mkataba wa kazi kati yake na Tip Top umeisha, kitu ambacho hakikuwa sahihi" Ninasikitika sana kwani katika wasanii ambao wamekuzwa vipaji vyao wakiwa Tip Top huyu ni mmojawapo, kwani hakuwa na kitu chochote".

"Lakini mpaka anaondoka kwetu alikuwa amejijenga na kutembelea gari, iliniuma sana kwani sikutegemea kama siku moja angeweza kufanya aliyoyafanya" anasema Tale na kuongeza kuwa kati yake na Z Anto hawakuwahi kugombana.

Licha ya matatizo yaliyotokea, Tale anasema kuwa msanii huyo hivi sasa amejitokeza na kuwasiliana na Bonge kwa njia ya simu akihitaji kurudi tena upya ndani ya kundi hilo.


PNC alikana msaada wangu
"PNC alifika toka Mwanza akiwa hana la kufanya, katika kipindi hicho chote alikuwa chini ya Mully B ambaye alikuwa akimsaidia sana kutokana na kipaji alichokuwa nacho.

"Baada ya kutaka kumsaidia niligundua kwamba hana pa kuishi hivyo niliamua kuishi naye katika nyumba yangu na nilikuwa nikilala naye kitanda kimoja mpaka pale nilipohitaji kuoa ndipo nilipomhamisha na aliendelea kuishi chumba kimoja na mdogo wangu.

"Lakini tabia zake zilianza kubadilika na baadaye nikaja kumsikia katika kipindi kimoja cha mahojiano akijieleza kwamba ameamua kujitoa Tip Top maana hakuna msaada wowote anaoupata na hajawahi kusaidiwa na mimi, niliumia sana.

Pingu ana majungu, mnafiki
"Kwa kweli nitasema kwamba Pingu ndiye aliyemshawishi Z Anto atoke ndani ya kundi, naye bila kufikiri akafuatana naye lakini hawakufika mbali wakabwagana.

"Baada ya kutoka alianza kuongea majungu mengi tu hii ilidhihirisha kwamba Pingu hakuwa mtu mzuri katika kundi kwani alikuwa unafiki.

Babu Tale anasema kwamba walikwenda Nairobi Kenya kwa ajili ya kurekodi Video na Juakali, kwa pesa zake lakini baada ya kutoka kwa wasanii hao walianza kumdai video hiyo ndipo yeye alivyoamua kuifuta.


Tale anasema kuwa licha ya yote waliyoyafanya mpaka sasa hakuna msanii ambaye alitoka nje ya kundi na bado anafanya vizuri, wengi wamerudi nyuma. Pia alisisitiza kwamba msanii kusimamiwa ni tofauti na akijisimamia yeye mwenyewe.

"Katika kundi tunafanya kazi kama 'Brothers' (ndugu) hivyo inakuwa rahisi wao kunizoea hivyo wanapofikia maamuzi mazito wanashindwa kunishirikisha.

Tale ni baba wa mtoto mmoja aitwaye Tale Junior huku akiwa na mkewe ambaye amekiri kumpenda kuliko mwanamke mwingine yeyote. Pia ni mdogo wa mwekezaji wa kundi hilo Abdi Bonge ambaye kwa hivi sasa amejiweka pembeni na kundi hilo na kuendelea na mambo yake mengine.

Kundi hilo hivi sasa lina vinara watano ambao bado wanakubalika katika ulimwengu wa muziki wa kizazi kipya kama Keisha, Tundaman, Madee, Cassim na Deso licha ya kuwepo wasanii wengine chipukizi.

Wednesday, May 12, 2010

JIDE AIBUKA KIDEDEA POLL YA ANKO MO BLOGSPOT!!

Katika shindano lisilo rasmi la kumsaka mkali wa bongo flava nchini Tanzania kwa upande wa wanawake lililokuwa likiendeshwa na Blog hii, hatimae limefikia mwisho huku Lady Jay Dee akiibuka kidedea kwa kupata kura takribani 45 ambazo ni sawa na asilimia 50.53.

Mshindi wa pili katika mchakato huo ni Keisher ambaye amepata kura 17 ambazo ni sawa na asilimia 17.89. Ray C ameshika narasi ya tatu kwa kura 16, huku K-ylln akishika nafasi ya nne kwa kura 16 na Best akishika mkia kwa kura 3.

Kura zote hizo zilipigwa na wadau wa VIJIMAMBO VYA TANGA kupitia Blog hii. Shukrani wote mliojitokeza na kuwapigia kura wasanii manowapenda kupitia Poll iliyokuwa hapo pembeni.

Nimewaletea changamoto nyengine ya kuchagua MKALI WA HIP HOP TANZANIA. Mpigie kura msanii unayedhani ni mkali zaidi ya wote kwa upande wa wanaume. Poll ipo hapo kulia!!

WAFAHAMU CELEBRITIES WA TANGA CITY!!!

Glory Chuwa, Miss Tanga 2010. Ambaye anamaliza muda wake mwaka huu.

Aliyevaa fulana ya njano ni Dj Bad Fuvu wa Mwambao Fm Radio, anayefuata ni Matonya msanii kutoka Tanga. Anayefuata ni Dula Maujanja, mtangazaji wa kipindi cha Tz Most Wanted kinachorushwa na Mwambao Fm, wa mwisho ni mkurugenzi wa 5 Brothers Entertainment inayoandaa Miss Tanga, Nassoro Makau.

Msanii Fady Dady kutokea Tanga, akiwa na Dj Bob Nass wa Breeze Fm Radio.

Mwandishi wa habari za michezo gazeti la Bingwa na pia mtangazaji wa Mwambao Fm Oscer Assenga aliyevaa miwani, akiwa na swahiba wangu- Ally Mohammed a.k.a Bra A wa Mwambao Fm pia.

Rass Bizzle...mkali wa Mic!

Tuesday, May 11, 2010

TUWAKUMBUKE MASHUJAA WETU WA TANGA!!!!!

Bwana Heri bin Juma (pia: bana Heri) alikuwa sultani wa Saadani iliyokuwa bandari ya biashara kwenye mwambao wa Bahari Hindi katika Tanzania kaskazini-mashariki tangu miaka ya 1870.

Mtawala wa Saadani

Alitawala chini ya Sultani wa Zanzibar kama mkubwa wake lakini akafaulu kutetea nafasi yake kama sultani aliejitegemea. 1882 aliweza kushinda jeshi la Sultani Sayyid Bargash aliyetaka kutawala Saadani moja kwa moja. Saadani kama miji mingine ya pwani ilifaidika na biashara ya Wazungu walioleta bidhaa na kulipa ushuru. Alielewana vema nao.

Kuja kwa Wajerumani

1886 Sultani Sayyid Khalifa wa Zanzibar alikodi eneo lake katika Tanganyika bara kwa Kampuni ya Kijerumani kwa Afrika ya Mashariki. Bwana Heri pamoja na viongozi wengine aliona amesalitiwa na Sultani hakuwa tayari kukubali utawala wa Wajerumani. 1888

Vita ya Abushiri

Bwana Heri aliunga mkono na upinzani wa Abushiri dhidi ya Wajerumani akipata usaidizi wa makabila wa eneo lake hasa Wazigua.

Alishambuliwa na kiongozi Mjerumani Hermann von Wissmann aliyekuwa na silaha za kisasa akapaswa kuacha kambi yake Saadani tar. 6 Juni 1889. Aliendela na vita ya msituni. Baada ya kushambuliwa tena na jeshi la Wajerumani katika Januari na Machi 1890 uwezo wake ulikwisha. Sayyid Khalifa aliwasiliana naye na Wissmann akatayarisha kujisalimisha kwake tar. 6 Aprili 1890. Wissmann aliyemheshimu Bwana Heri hakumwua kama Abushiri bali akamwambia kujenga Saadani upya.

Upinzani wa wenyeji ulishindwa lakini ulisababisha mwisho wa utawala wa kampuni iliyoshindwa kukandamiza uasi wa Waafrika. Serikali ya Ujerumani iliona haja ya kungilia kati na kuchukua utawala wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani mkononi mwaka kama koloni ya serikali ya Ujerumani.

Mwisho wake

Mwaka 1894 alijaribu tena kupambana na Wajerumani lakini alishindwa kwa mara ya pili. Akaondoka bara kwenda Zanzibar alipokufa baadaye.

LIBENEKE MPAKA INDIA!!!!!!!

Mtanzania huyu anaitwa Ally Shaaban, yupo nchini India anaendeleza libeneke kupitia blog yake ya www.allyshams.blogspot.com inayojihusisha na maswala ya jamii. Itembelee uone matukio tofauti ya ndani na nje ya India.

Monday, May 10, 2010

'PASTOR'- NGOMA MPYA YA ROMA!!

Mkali wa Hip Hop kutokea Tanga City Rymes Of Magic Attractio ama ROMA, ameachia ngoma yake mpya inayokwenda kwa jina la Pastor. Ngoma hiyo ambayo ameitengeneza pale Tongwa Record, imebeba maneno ya kiroho yenye kuletea upako na kurudisha wokovu kwa waliopotea na Roma mwenye ndio Pastor!!

Wimbo unaanza hivi- "I am the pastor of this church, i am the pastor of this churh......Fanya ishara ya msalaba upokee haya maubiri, mimi ni mteule ninawaletea injili, nina ushuhuda wa kiroho bwana yu aja msubiri, natangaza UPAKO na habari za mnara wa Babeli"

Kama vipi unaweza kuusikiliza hapo juu palipoandikwa SIKILIZA TANGA FLAVA HAPA! Tayari Roma anatamba na ngoma zake kama Salute, Tanzania pamoja na Mr President ambayo hadi sasa bado inafanya vizuri karibu kila redio nchini Tanzania.

Roma pia ametajwa kwenye Teen Extra Award category ya 15. Lyricist Of The Year ambapo anachuana na wasanii wengine kama Fid Q, Niki Wa Pili, Ngwea, Joh Makini, Jay Moh na G Nako. I know Tanga tunaweza na ROMA ndie msanii pekee anayestahili kuwa Lyricist wa mwaka kutokana na tungo za ukweli zinazopatikana kwenye ngoma zake zote!

Unachotakiwa kufanya ni kufungua hii website http://www.nipe5.com Utakapoifungua angalia mkono wako wa kushoto kuna sehemu imeandikwa Teen Extra Award hapo utabonyeza kwa ajili ya kuona washiriki wote halafu utaingia kipengele cha 15. Lyricist Of The Year na hapo utabonyeza jina la ROMA.

Au kuingia moja kwa moja kwenye hiyo web site na kumpigia kura Roma Bonyeza Hapa

NITADAI CHANGU HADI KIAMA- SUMA LEE

Msanii kutoka Tanga Suma lee juzi alifanya mahojiano na kituo cha redio cha East Africa -Katika mahojiano hayo Suma aliulizwa kuhusiana na wimbo wake unaoitwa Driving Crazy aliomshirikisha Quick Rocka mbona hajaufanyia video na nimkali sana.

Jamaa akafunguka na kuelezea ukweli wote ya kwamba alikuwa hana hela na alipomfuata Adamu wa Visul Lab alimwambia anataka video na Adamu akamwambia ni shs laki 9, so Suma yeye akamwambia anatanguliza laki mbili halafu anampa tena laki 3 ndio waanze kushoot itakapoisha atammalizia laki 5 zake.

Cha ajabu anachosema Suma Lee baada yakumpa hiyo hela akawa anamcheki jamaa hapokei simu yake wala nini lakini akimtumia msg za dini hata kama imemfikia nusu Adamu anamjibu tuma tena imekuja nusu lakini swala la kushoot jamaa analipotezea.

Alipoulizwa sasa vipi hiyo hela utamsamehe au inakuwaje..? jamaa alijibu
"hiyo hela nitaidai mpaka kiama, laki mbili nyingi ndugu yangu lazima ataitoa tu"

Mwishoni akasema video hiyo atampatia rafiki yake Kallage ili aifanye na isipotee hivi hivi, kuhusu swala la album Suma alisema album inakaribia kuisha na itakuwa na nyimbo 10 na jina la album itaitwa HESABU ZA MAPENZI, na mtu mzima Marco Chali kutoka MJ Rec ndio ataisimamia kila kitu mpaka iwe sawa kuingia sokoni.

Friday, May 7, 2010

Thursday, May 6, 2010

MISS NGAMIANI 2010 HIYOOOO!!!

Ijumaa ya tahere 28/05/2010, kunako uwanja wa Mkwakwani. Dont Miss!!!!

NAVAA VIMINI KUONGEZA MVUTO- JIDE

Anaitwa Jide, Lady Jaydee au 'Manka' kama anavyopenda ajulikane siku hizi..ameweka bayana kwamba anapendelea zaidi kuvaa vimini ili kuongeza mvuto na kusisimua mashabiki wake anapokuwa jukwaani.

Lakini hakuishia hapo msanii huyo ameliambia gazeti moja maarufu la nchini Kenya kuwa hapendi kurudia nguo kwa vile anawaogopa mapaparazi.

"Napenda kuvaa nguo fupi kwenye maonyesho na viatu virefu. Nywele zangu pia nazibadili kwa mitindo tofauti kila siku," alisisitiza msanii huyo anayemiliki Machozi Band inayotamba Dar es Salaam.

"Kinachonifanya nionekana tofauti na wasanii wenzangu ni kwamba ninajituma sana na ninapenda sana kutengeneza nywele zangu, ni nadra sana kunikuta kwenye staili moja ya nywele wiki mbili nzima."

"Kujirefusha huwa navaa viatu virefu wakati ninapokuwa jukwaani na magauni au sketi fupi ili miguu ionekane mirefu. Napenda sana staili za mitaa."

Wednesday, May 5, 2010

ZANTEL YADHAMINI ZIARA YA MPIRA MAALUMU WA KOMBE LA DUNIA TANZANIA

Naibu Waziri wa Habari Michezo na Utamaduni Mheshimiwa Joel Bendera akitia saini mpira maalum wa kombe la dunia katika sherehe za kuukaribisha rasmi mpira huo nchini Tanzania. Kushoto kwake ni Bw. William Mpinga, Meneja Masoko wa Zantel. Zantel ndio wadhamini wakuu wa ziara ya mpira huu hapa nchini.

Meneja Masoko wa Zantel Bw. William Mpinga akitoa hotuba kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Zantel kwenye sherehe za kuukaribisha rasmi mpira maalum wa kombe la dunia iliofanyika leo katika viwanja vya Karume jijini Dar es Salaam. Zantel ndio wadhamini wakuu wa ziara ya mpira huu hapa nchini.

Meneja Masoko wa Zantel Bw. William Mpinga naye akiweka saini yake kwenye mpira maalum wa kombe la dunia kwa niaba ya Zantel ambao ni wadhamini wakuu wa ziara ya mpira huo nchini Tanzania

Tuesday, May 4, 2010

FAIDIKA NA WANAUME HALISI!!!!!!!!!

Kwa wale wapenzi wa kundi la TMK Wanaume Halisi, mnaambiwa kuanzia sasa kila mpenzi anaweza kujiunga na kundi hilo na kuwa mwanachama wa kudumu.

Unachotakiwa kufanya ni kutuma sms yenye neno KIUMENI kwenda namba 15551.

Je kuna faida gani ya kuwa mwanachama wa tmk wanaume halisi?

1. Utakuwa mtu wa kwanza kujua kitu gani kinaendelea kwenye kundi kabla ya kujuzwa na vyombo vya habari.

2. Utapata punguzo la asilimia 20 kwenye kila bidhaa itakayouzwa na tmk wanaume halisi kuanzia tshirt,tape,cd au kiingilio cha kwenye show zao.

3. Pia kama mwanachama utakuwa na fursa kubwa ya kutoa mchango wa mawazo au maoni kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza kundi.


NGOMA MPYA KUTOKEA TANGA!!!

Anaitwa Untouchable, msanii kutokea Tanga City! Sikiliza wimbo wake mpya ambao unafanya vizuri hivi sasa kunako redio tofauti tofauti nchini Tanzania, unaitwa 'Binadamu' amemshirikisha Kassim.

Kochas kutoka Omega Boys ya jijini Tanga, sikiliza ngoma ya Omega hapo juu palipoandikwa SIKILIZA TANGA FLAVA HAPA! Ngoma mpya inaitwa 'Kama Nyota" ambayo wamemshirikisha Dully Sykes!

Monday, May 3, 2010

MLELA AJITOA SEREBUKA!!!!!

Star kunako industry ya Bongo Movies,Yusuf Mlela ‘Angelo’, amejitoa kwenye Kinyang’anyiro cha kipindi cha 'Serebuka' ambacho huwa kinachukua nafasi every Tuesday pale Club ya kimataifa ya Billicanas, jijini Dar na kurushwa hewani na Kituo cha Televisheni cha TBC1 kila Jumapili.

Akielezea sababu ya kujitoa kwake, Mlela ana-reveal kwamba sababu kubwa ya kuchukua uamuzi huo inatokana na kuhisi kuwa ndani ya mpambano huo kuna mizengwe na kwamba kuna uwezekano mshindi amekwishaandaliwa.



“Truly nahisi kama kuna mizengwe inaendelea na si ajabu mshindi amepangwa. Kwa mfano wiki iliyopita kabla sijajitoa majaji walinilazimisha nicheze wimbo ambao sijaufanyia mazoezi kwa madai kwamba ule niliokuwa nimeufanyia mazoezi umeshachezwa na mshiriki mwingine, hiyo ni sababu nyingine ambayo ilinifanya nihisi nachezewa rafu.” –alisema Mlela.

NEEMA JAMAL NDIO MISS CHUMBAGENI 2010!

Hatimaye mrembo Neema Jamal,juzi alifanikiwa kulitwaa taji la Miss Chumbageni 2010 baada ya kuwabwaga warembo wengine 7 waliokuwa wakiwania taji hilo.

Mashindano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa La Club Tanzanite Chuda Relini jijini Tanga na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa watazamaji.

Mashindano hayo ambayo yalipambwa na burudani ya muziki kutoka bendi ya Bwagamoyo International inayoongozwa na Mwinjuma Muumini 'Kocha wa Dunia'.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Halima Salehe wakati nafasi ya tatu ilikamatwa na Chausiku Ibrahimu huku Taji la Kipaji likinyakuliwa na Agnes Mambo ambaye pia ni Mtangazaji wa Radio Mwambao Fm ya jijini Tanga.

Mashindano hayo yalikuwa ya ushindani mkubwa kutokana na warembo hao kuwa na vigezo vinavyokaribiana huku Agnes Mambo akiongoza kwa kushangiliwa na mashabiki waliohudhuria onesho hilo.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Onesho hilo,Sussan Uhinga kutoka Kampuni ya Apple Partners mshindi wa kwanza alijinyakulia kitita cha shilingi 100,0000 huku mshindi wa pili na watu wakijinyakulia sh 50,000 huku washiriki wengine wakipata kifuta jasho cha sh.30,000 kila mmoja