MIONGONI mwa suala yanayotishia uhai wa viumbe na mimea duniani hivi sasa ni suala la mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa kwa ujumla. Mabadiliko hayo chanzo chake kimetokana na uharibifu wa mazingira asilia unaoendelezwa na binadamu wakati anapojishughulisha ili kutafuta maendeleo pasipo kuzingatia kanuni za uasilia. Matokeo ya jumla ya shughuli hizo ni kuongezeka kwa joto duniani linalosababishwa na kasi ya uzalishaji wa gesi ya ukaa katika anga na kuathiri uhai wa Binadamu, viumbe hai wengine na mimea pia.
Athari kubwa itokanayo na mabadiliko ya Hali ya Hewa ni kupanda kwa kiwango cha joto duniani ambako husababisha mabadiliko katika nchi na kuleta matukio yenye athari hasi kwa binadamu kiuchumi na kijamii. Athari mbalimbali zimeendelea kuonekana katika maeneo tofauti tofauti duniani ikiwemo hapa Tanzania na kuanza kufifisha matumaini ya kiuchumi ya wananchi wengi katika maeneo mbalimbali hasa ikizingatiwa kwamba wengi kati yao wanategemea sana shughuli za kilimo na uvuvi kupata kipato.
Pamoja na mambo mengine kimsingi zimepunguza kasi ya utekelezaji wa shughuli muhimu za kiuchumi ambazo katika maeneo mengi zimekuwa zikitegemea uwepo wa bahari, mito na maziwa, mvua za uhakika pamoja na misitu. Matokeo ya mabadiliko hayo yamevuta hisia tofauti kwa taifa na wanaharakati mbalimbali wa mazingira kuanza kujaribu kuhamasisha jamii kupunguza shughuli hasi za kiuchumi na kijamii kwa mazingira kama mbinu ya kupunguza kasi ya vitendo vinavyochochea.
Kutokana na uzito wa matokeo hayo Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, kwa kushirikiana na wanaharakati wa masuala ya mazingira imeanzisha kampeni maalumu ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kama njia ya kukabili tatizo. Lushoto ndiyo wilaya pekee katika mkoa wa Tanga iliyokuwa ikiongoza kwa kuwa na msimu mrefu wa baridi kwa mwaka, ikilinganishwa na maeneo mengine ya wilaya saba zilizosalia ambazo kwa pamoja zinaunda mkoa huo. Wenyeji wa wilaya hiyo wanabainisha kwamba ilikuwa ni jambo la kawaida kwa Mvua ya Barafu kunyesha kwenye maeneo mengi ya wilaya hiyo.
Hapakuwepo na msimu wa joto kutokana na uwepo wa misitu minene, iliyokuwa imefunika Tao la Milima ya Usambara Magharibi. Wanasema ni katika miaka ya hivi karibuni ndipo waliposhangaa kuona hali ikianza kubadilika na kushuhudia ukame unavyokausha mazao katika baadhi ya mashamba, kuanza kwa msimu wa joto ambao awali haukuwepo kabisa sambamba na idadi kubwa ya wananchi kuugua ugonjwa hatari wa Malaria unaoenezwa na Mbu ambao wanapenda kuishi zaidi kwenye maeneo yanye joto kali.
Wanasema hayo yote ni matokeo ya wananchi kujihusisha na shughuli za kijamii na kiuchumi kama vile uchomaji ovyo misitu, ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, kuchoma mkaa, mbao na magogo, kilimo katika vyanzo vya maji pamoja na uchimbaji wa madini shughuli ambazo licha ya kuwaongezea kipato, sasa zimewatumbukia nyongo na kuanza kuwataabisha. Tegemeo kubwa la wakazi wa wilaya ya Lushoto ni kilimo cha matunda, mboga mboga na biashara ambavyo tayari vimeanza kuathiriwa na mabadiliko hayo ya tabianchi.
Majira ya mwaka yanabadilika kiasi kwamba ratiba ya mvua haieleweki, hasa kwa vile wakati na kiasi cha mvua za masika na vuli kunyesha hakitabiriki kutokana na ujio wa Kiangazi ambacho sasa kimeingia kwa kasi katika maeneo mengi ya wilaya hiyo na kusababisha jua kuwa kali badala ya baridi na mvua za barafu. Aidha, shughuli za kijamii ikiwemo kuongezaka kwa idadi ya watu ambao wanahitaji maeneo zaidi ya makazi na kilimo kwa namna moja au nyingine kumechangia matokeo hayo kutokana na ukweli kwamba ujenzi wa makazi unahitaji ardhi pamoja na rasilimali misitu ili kukamilisha makazi.
Kutokana na kupanuka kwa mji na makazi kumeshawishi ongezeko la mahitaji ya kupata nishati ya uhakika kwa ajili ya kupikia ikiwemo kuni na mkaa yameongezeaka wilayani humo hali ambayo kidogo kidogo inaendelea kuchochea uharibifu wa mazingira hasa katika misitu. Hivyo basi, Katika kukabiliana na changamoto hizo za uharibifu wa mazingira taasisi isiyo ya kiserikali kwa kushirikiana na Halmashauri hiyo ya wilaya wanatekeleza Kampeni hiyo maalum ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuhamasisha jamii kupunguza athari hasi kwa kusisitiza matumizi ya Nishati Mbadala kwa kupikia.
Kampeni hiyo ki msingi inalenga kuwaelimisha wananchi wa wilayani humo namna ya kupokea mabadiliko hayo na kutafuta mbadala wa matumizi ya nishati za kuni na mkaa kuanzia ngazi ya kaya ili kusaidia kuwajengea wananchi uwezo zaidi kwa sababu bado wanategemea kuendesha maisha kwa kutumia uwepo wa misitu ya milima ya Usambara. Kupitia kampeni hiyo, wananchi wanaelewesha sera zilizopo, faida na umuhimu wa kutunza mazingira kwa kuhimiza matumizi ya nishati ya mkaa mbadala wa kupikia maarufu kama mkaa tufe (briquettes), tofauti na mazoea yaliyojengeka miongoji mwa jamii ya watanzania ya kutumia kuni na mkaa kupikia.
Ili kuhakikisha kampeni hiyo inafanikiwa na kuenezwa katika maeneo mengi ya mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla Wanaharakati hao wa masuala ya Mazingira ambao ni Kampuni ya Environmental Engineering (EEco) Ltd, inaanzisha kiwanda cha kutengeneza kwa wingi Mkaa Tufe mjini humo. Aina hiyo ya nishati itakayozalishwa na kiwanda hicho, haina tofauti na ile inayotengenezwa sasa na baadhi ya vikundi vya wanawake wajasiriamali wadogo walioko wilayani humo, ambao awali walipatiwa teknolojia hiyo na kuanza kuzalisha mkaa tufe kwa matumizi ya kaya katika vijiji wanamoishi. Mkaa tufe uwezo mkubwa wa kuhifadhi mazingira kutokana na kumudu kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kuni na mkaa nyumbani tofauti na hali ya mahitaji ilivyo sasa katika kaya nyingi za wilayani humo na katika makazi yaliyoko mjini.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo yenye makazi yake wilayani hapa, John Nshunju, akizungumza kwenye mahojiano maalum hivi karibuni amesema mkaa tufe ni rahisi kwa kuwa unatengenezwa kwa kutumia teknolojia rahisi ya kuchanganya takataka za shambani, majani, karatasi, vumbi la mbao au mpunga na maji kwa kutumia mashine maalumu iitwayo ‘divider’. “Ni aina ya mkaa tofauti na ule ambao tumezoea kuuona, Mkaa Tufe unaundwa katika umbo la vipande vya mviringo vyenye tobo katikati ili kuruhusu hewa kupita kwa urahisi wakati wa kuuchoma, mkaa huu unafaa kutumiwa kwenye jiko la aina yoyote likiwemo la kuni,” anaeleza.
Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa kipande kimoja cha mkaa huo, ambacho kwa sasa kinauzwa kwa bei ya Sh 100 kina uwezo wa kumudu kuchemsha chai inayotosha kunywewa na watu watatu kwa wakati mmoja na kudai nishati hiyo licha ya kuboresha mazingira inasaidia kupunguza gharama za fedha kwa ajili ya kununua mkaa kwa matumizi ya kaya kwa siku. “Mkaa tufe pamoja na kutumika kuhifadhi mazingira pia unasaidia kupunguza gharama za kununua mkaa na kuni nyumbani mathalani kwa wastani kwa siku moja hapa Lushoto familia inauwezo wa kutumia mkaa wa kati ya Sh 800 hadi Sh 1,000 kupikia chakula cha familia lakini kwa kutumia vipande vinne tu vya mkaa tufe vinamtosheleza mama kuandaa chai na chakula cha familia ikiwemo kuchemsha maharage yanayoweza kuliwa na watu wanne,” anasema.
Anasema tangu kuanzishwa kwa Kampuni hiyo miaka mitano iliyopita, wamefanikiwa kufundisha na kuwezesha mtaji midogo kwa vikundi vitatu vya wanawake, ambayo kwa kutumia mashine ndogo za mkono sasa wanazalisha na kuuza mkaa tufe kwa jamii zinayowazunguka. Kampuni ya Environmental Engineering (EEco) Ltd inaamini kwamba kupatikana kwa kiwanda hicho Lushoto, kutaongeza uzalishaji mara dufu wa nishati hiyo ili baadaye iweze kufikia wananchi wengi zaidi, kwa sababu malighafi ipo nyingi na inapatikana bure.
No comments:
Post a Comment