BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX

Thursday, February 17, 2011

TANGA YAONGEZA UZALISHAJI WA CHAKULA

MKOA wa Tanga umefanikiwa kuongeza zaidi ya tani 374, 118 za chakula zinazotosheleza mahitaji ya wakazi wake kwa mwaka 2010/2011.

Hatua hiyo imetokana na wananchi kwa kushirikiana na wataalamu wa kilimo kuhamasika na kuaongeza uzalishaji wa mazao hayo baada ya mavuno ya ndizi na majimbi kubadilishwa na kuwa katika hali ya ukavu na kufikia tani 903,222.

Ofisa Kilimo wa Mkoa, Lameck Tungu alisema hayo wakati akiwasilisha mada ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2009/2010 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika jijini hapa.

Alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, hali ya chakula katika halmashauri zote tisa za mkoa huu ilikuwa nzuri kutokana na kutokuwepo kwa maeneo yaliyopata upungufu wa chakula tofauti na mwaka juzi.

“Mwaka jana katika msimu wa kilimo wa masika, tulilenga kulima na kutunza mazao ya chakula katika hekari 556,326 ambazo zilikadiriwa zitoe mavuno ya chakula ya tani 1,316,812.

Hadi kufikia mwisho wa msimu huo, mkoa ulikuwa umelima na kutunza hekari 429,095 ambazo zimetoa tani 951,928 sawa na asilimia 72 ya uzalishaji uliolengwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Tungu, mkoa huo unakadiriwa kuwa na wakazi 1,858,492 na hivyo mahitaji ya chakula kwa kiwango cha juu cha kujitosheleza katika msimu wa mwaka huu ma wavuno yanakadiriwa kufikia tani 529,104.

“Tunaamini chakula cha ziada kitasaidia kutosheleza mahitaji ya wakazi iwapo tu watakitumia kwa uangalifu mkubwa, tunawashauri waepuke uuzaji holela, wakihifadhi vizuri na wasijaribu kukitumia kwa shughuli za kutengeneza pombe za asili,” alifafanua Tungu.

Alisema pamoja na uzalishaji huo, tathmini ya hali ya chakula inaonesha kuwa wakazi wa vijijini takriban 69,585 wamezalisha chakula cha kutosheleza mahitaji yao ambayo ni tani 19,710 huku wakazi wengine wapatao 221,480 wa mijini ambao jumla ya mahitaji yao ni tani 63,072 wakikabiliwa na upungufu wa chakula.

Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, aliwataka wajumbe hao kuhakikisha chakula kinahifadhiwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza uhakika wa chakula.


Na Anna Makange, Tanga


No comments:

Post a Comment