BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX

Monday, February 28, 2011

WATENDAJI WA VIJIJI, MITAA KOROGWE WAZEMBE KUKIONA!


MKUU wa wilaya ya Korogwe, Erasto Sima amewataka wananchi kumtaarifu juu ya watendaji wa serikali za vijiji wanaokiuka sheria na taratibu kwa kushindwa kuitisha mikutano mikuu ya vijiji.

Ametoa agizo hilo baada ya kukabidhi baiskeli 122 zenye thamani ya Sh milioni 15.2 kwa watendaji wa vijiji vinavyounda Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kupitia mradi wa kusaidia utekelezaji wa utawala bora katika serikali za mitaa.

Mradi huo unafadhiliwa na Mpango wa Ushirikiano wa Ujerumani na Tanzania wa kuimarisha utawala bora ngazi ya jamii (SULGO-GIZ).

Alisema ukwepaji wa kuitishwa kwa mkutano mkuu wa kijiji au mikutano mingine ya kawaida ikiwemo ya kutoa taarifa za mapato na matumizi ya kijiji unaofanywa na baadhi ya watendaji katika serikali za vijiji ni ishara ya wazi ya ukiukwaji wa misingi ya utawala bora katika jamii.

Alisema wananchi wana wajibu wa kumpa taarifa awashughulikie watendaji wa namna hiyo.

“Nimejulishwa kwamba pamoja na msaada huu wa baiskeli mradi wa SULGO-GIZ tayari umewajengea uwezo kuhusu majukumu na uwezo wa halmashauri za vijiji ikiwemo kanuni za kuandaa, kuendesha mikutano mbalimbali ya vijiji,” alisema na kuongeza:

“Mikutano hiyo iwasaidie kuandaa bajeti na mipango ya maendeleo kwa lengo la kuhakikisha misingi ya utawala bora naya kidemokrasia na isimamiwe ipasavyo ili kuharakisha maendeleo lakini kinyume na matarajio, baadhi yenu bado mnaendelea kulalamikiwa na wananchi kwamba hamuitishi mikutano inavyostahili na kusababisha wananchi kuchelea kushiriki kuchangia maendeleo yao”.

Mkuu huyo alisema hatasita kumchukulia hatua za kinidhamu Ofisa Mtendaji yeyote wa kijiji na kata ambaye atabaini kuwa ameshindwa kusimamia misingi ya utawala bora.

Aliwataka watendaji hao kutumia baiskeli kuwafikia wananchi katika vitongoji mbalimbali wakati wa kuhamasisha, kutekeleza miradi ya maendeleo na hasa wanapoanza maandalizi na kusambaza taarifa za mikutano ya kijiji.

Na: Anna Makange
, korogwe

No comments:

Post a Comment