Ricardo Izecson dos Santos Leite "KAKA"- MLOKOLE ANAYETANGAZA INJILI KWENYE SOKA.
Kama utazungumzia wachezaji ambao wamepata mafanikio zaidi kwenye ramani ya soka duniani, hasa kwenye timu ya taifa ya Brazili na klabu ya Ac Milan ya nchini Italia. Basi hutasita kumtaja mshambuliaji Ricardo Izecson dos Santos Leite, wengi humfahamu kama 'Kaka'.
Alizaliwa mnamo April 22 mwaka 1982 huko nchini Brazili kwenye mji mkuu wa nchini hiyo Brasilia. Ni mshambuliaji mwenye umri wa miaka 26 kwa sasa, na pia ana urefu wa futi 6.
Kwa sasa mchezaji huyo anachezea klabu ya Ac Milan ya nchini Italia akiwa anavalia jezi namba 22. Kipaji chake kilianza kuchomoza akiwa na timu za vijana wadogo wakati huo akiwa na miaka minane tu.
Pia alikuwa akicheza na vijana wenzake katika klabu ya Sao Paulo hata kufanikiwa kuwamo katika kikosi cha pili na alipofikia umri wa miaka 15, alisaini mkataba na kikosi cha vijana wa SPFC kwa ajili ya michuano ya Copa de Juvenil.
Kutokana na kiwango chake, mwaka 2001, Kaká alipandishwa katika kikosi cha kwanza na kufanikiwa kutikisa nyavu mara 12 katika mechi 27, hivyo kuwa mfungaji bora wa São Paulo na kuibebesha ubingwa.
Katika msimu uliofuata, Kaka alifanikiwa kupiga bao 10 kwenye mechi 22 za ligi hiyo na ndipo hapo alipoanza kutakiwa na klabu kubwa barani ulaya.
Klabu ya AC Milan, ikiwa bingwa wa ligi kuu ya Italia msimu wa mwaka 2003, ndipo ilipoamua kumnunua Kaka kwa kitita cha dola mil. 8.5 za Marekani kwa mapendekezo ya mmiliki wa klabu hiyo, Silvio Berlusconi.
Punde tu alipotinga kwenye kikosi cha timu ya Milan, Kaka alionekana kuwa na hamasa kubwa ya mafanikio kwani katika mechi ya kwanza ya ligi kuu nchini humo maarufu kama Serie A- Ac Milan iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ac Ancona.
Kuhakikisha kuwa uwezo wake ni mkubwa kisoka, hadi mwisho wa msimu huo- Kaka aliweza kuondoka na mabao 10 kwenye mechi 30 alizocheza na hatimae kuibebesha kombe la Scudetto klabu yake hiyo halikadhalika ubingwa wa Super Cup barani ulaya.
Aidha, Kaká alikuwa miongoni mwa washambuliaji watano wakali kwenye msimu wa mwaka 2004/2005, akiwa nyuma ya kinara wa mabao wa msimu huo, Andriy Shevchenko.
Zaidi ya hapo mchezaji huyo pia alifunga mabao saba katika mechi 36 kwenye ligi ya Serie A, wakimaliza kwa kuwa nyuma ya Juventus.
Kwa msimu huo huo wa mwaka 2004/05, Ac Milan ilipata pigo kwa kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Ulaya kwa kufungwa kwa mikwaju ya penati na timu ya Liverpool ya nchini Uingereza.
Hata hivyo, pamojana na Ac Milan kukosa ubingwa huo, Kaka aliweza kuchaguliwa kuwa mshambuliaji bora wa mashindano hayo na kumaliza msimu huo kwa kutwaa tuzo ya Ballon D’Or.
Msimu uliofuata wa mwaka 2005/2006, Kaka aliipigia timu yake mabao matatu kwenye mechi moja yaani 'Hat-Trick kwenye mashindano ya nyumbani.
Aprili 9, 2006, aliifungia tena mabao matatu klabu yake dhidi ya Chievo Verona. Mabao hayo aliyapiga katika kipindi cha pili cha mchezo.
Baada ya Shevchenko kuikacha klabu hiyo na kuchukuliwa na klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza, msimu wa mwaka 2006/2007 ulionekana bora sana kwa mchezaji Kaka baada ya kuweza kumudu nafasi ya kiungo na mshambuliaji.
Msimu huo huo ulimalizika kwa mchezaji huyo kuwa mfungaji bora wa ligi ya mabingwa barani ulaya maarufu kama Uefa Champions League huku akiiwezesha timu yake kutwaa ubingwa wa michuano hiyo migumu barani humo.
Hata hivyo moja kati ya mechi ambazo zimebaki kuwa ni historia nzuri kwa mchezaji huyu, ni ile dhidi ya Manchester United ambapo ilimlazimu kocha wa timu hiyo Sir Alex Ferguson kumpa pongezi kocha wa Milan Carlo Ancelotti baada ya timu yake kuisambaratisha United kwa jumla ya mabao 3-0 kwenye nusu fainali ya klabu bingwa barani ulaya.
Pongezi hazikumfikia kocha wa timu hiyo pekee, aidha Ferguson alikiri kuwa Kaka, ni miongoni mwa wachezaji bora kwenye ramani ya soka duniani kwa mwaka huo.
Kilichofuata baada ya mechi hiyo, ni Kaka kutajwa kama mchezaji bora wa dunia na jarida la michezo la Italia, liitwalo Gazzetta dello Sport.
Juni mwaka 2008, gazeti la michezo la nchini Ujerumani la Kicker, lilimtaja Kaka kama mchezaji bora wa dunia akifuatiwa na Cristiano Ronaldo na Ronaldinho ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Ac Milan.
Tuzo nyengine ambazo Kaka amezinyakua hadi sasa ni pamoja na ile ya Revista Placar Bola de Ouro mwaka 2002, Mchezaji bora wa Campeonato kwa mwaka 2002 pia. Alichukua pia tuzo ya mchezaji bora wa Kombe la CONCACAF kwa mwaka 2003.
Mwaka 2005 alichukua tuzo ya kiungo bora wa UEFA Champions League, na mwaka 2006 alinyakua tuzo ya mchezaji bora wa kigeni kwenye ligi ya Seria A nchini Italia.
Haikuishia hapo tu, Kaka alichukua tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Fifpro kwa mwaka 2007 na pia mshambuliaji bora wa ligi kuu barani ulaya kwa mwaka huo huo wa 2007.
Alipewa tuzo ya mpira wa dhahabu kwenye kombe la dunia la klabu, pia alitunukiwa tuzo ya kampuni ya Toyota na ile ya Ballon d’Or- yote hiyo ikiwa ni mwaka 2007.
Huyu ni kiungo mahiri wa mabingwa wa soka Ulaya na dunia nzima kwa ujumla, ambaye licha ya kuibuka mchezaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia ametwaa tuzo ya uchezaji bora wa dunia mwaka 2007.
Hivyo, ingawa kila mchezaji amepata mafanikio kulingana na alivyojituma na kujaliwa na Mwenyezi Mungu, lakini huyu ndiye aliyefanikiwa zaidi, japokuwa kuna wengine waliofuatia.
Hao ni kama Christian Ronaldo wa Manchester United ya nchini Uingereza, Samwel Eto’o wa Barcelona ya Hispania, Didie Drogba Chelsea, Fernando Torres wa Liverpool pamoja na Raul Gonzalez wa Real Madrid.
Baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa dunia kwa mwaka huo wa 2007, Kaka alikaririwa akisema kuwa:
“Namshukuru Mungu kwa kuwa karibu nami, namshukuru mke wangu, mwanangu na kikosi changu cha Ac Milan pamoja na mashabiki wote wa Ac Milan na Brazil kwa kufanikisha kushinda tuzo hii,” a
Kaka alisema pia, kibinadamu unaweza kumwomba Mungu hiki na kile, lakini kwa mapenzi ya Mungu, anaweza kukujalia zaidi hata ya kile ulichoomba.
Nyota huyu anamaanisha kuwa, yeye aliomba siku moja aje kuwa mchezaji mahiri, lakini Mwenyezi Mungu amemjalia zaidi hata ya alichoomba.
Katika dirisha dogo la usajili la Januari mwaka huu wa 2009, Kaka aliweza kukataa mabilioni ya klabu ya Manchester City ya nchini Uingereza baada ya klabu hiyo kutaka kumchukua kwa kitita cha pauni milioni 100.
Endapo mchezaji huyo angekubali dau hilo, ndio angekuwa mchezaji wa kwanza kununuliwa kwa pesa nyingi kwenye historia ya wachezaji walionunuliwa kutokea ligi kuu nchini Italia.
Katika maisha yake ya kawaida, Kaka ni mtu aliyeokoka na anampenda mungu kikweli. Mara nyingi kwenye mechi ambazo anacheza na kufanikiwa kufunga goli, ndani huvaa fulana inayoonyesha maneno ya mungu.
Kwa mfano mwaka 2005 wakati timu yake ya taifa ya Brazili ilipocheza na Argentina kwenye mchezo wa kirafiki, Kaka aliionyesha fulana yake ya ndani iliyokuwa na maneno "JESUS LOVES YOU' baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa magoli 4-1.
Mwaka 2005 Kaka alifunga ndoa na Caroline Celico mwenye umri wa miaka 23 kwa sasa, ndoa ilifungwa huko nchini Brazili kwenye mji wa Sao Paulo. Hadi sasa wanandoa hawa wamebahatika kuwa na mtoto mmoja Luca Celico Leite aliyezaliwa Juni 10 mwaka 2008.
Jina la Kaka alilipata kwa kaka yake anayeitwa Rodrigo ambaye pia ni mwanasoka, kwa sasa anachezea klabu ndogo huko nchini Brazili ya Alphavile- alizoea sana kumuita "Caca", baadae akawa anamuita Ricky na mara ikabadilika na kuitwa KAKA jina lililozoeleka hadi hii leo kwenye ramani ya soka ulimwenguni kote.
KAKA NA TIMU YA TAIFA YA BRAZILI
Kaká alianza kuonekana kwenye kikosi cha Brazil mwaka 2002, siku ilipokutana na Bolivia.
Alikuwa mmoja wa wachezaji walioiwezesha timu ya Brazil kuchukua Kombe la Dunia mwaka 2002 kwa kuifunga Ujerumani 2-0 katika fainali hizo.
Akiwa chini ya kocha Luize Felipe Scolari kipindi hicho, Kaka aliweza kucheza kwa dakika 25 tu kwenye michuano hiyo hiyo wakati Brazili ilipokutana na Costa Rica.
Mwaka 2003, Kaká aliteuliwa kuwa nahodha katika michuano ya Kombe la Dhahabu, ambako Brazil ilimaliza ikiwa bingwa huku Kaka akiwa wa pili kwa ufungaji kwa kupiga mabao matatu.
Juni 29, 2005, aliisaidia timu yake kuitandika Argentina 4-1 katika mechi ya CONCACAF.
Mwaka 2004, Kaka alimaliza huku akipigiwa kura na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa mwaka huo.
Mwaka 2006, Kaká aliipaisha timu yake kwa kuifungia bao la pekee katika mechi ya ufunguzi walipoifunga Crotia katika michuano ya fainali za Kombe la Dunia mwaka huo.
Kaka, aliendelea kuwa mchezaji mzuri hadi pale walipoondolewa na timu ya Ufaransa kwenye robo fainali za Kombe la Dunia.
Septemba 3, 2006, aliifungia Brazil bao ambalo liliwajengea heshima na kufuta uteja kwa timu ya Argentina, iliyo pia Amerika ya Kusini.
Mei 12, 2007, Kaka aliachwa kwenye kikosi cha Brazil kilichoshiriki Kombe la Copa Amerika baada ya nyota huyo na Ronaldinho Gaucho kusema walihitaji kupumzika.
Baada ya kikosi hicho cha timu ya taifa kuchukuliwa na aliyekuwa beki wa zamani wa timu hiyo Carlos Dunga, aliamua kumrejesha Kaka katika kikosi chake baada ya kupigiwa kelele na mashabiki.
Kaká, aliitwa kwenye kikosi hicho na kucheza dakika 70 siku Brazil ilipotoka sare ya 1–1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Uingereza Juni mwaka 2008.
Alikuwamo pia katika kikosi cha Brazil ambacho Juni 5, kilitoka sare ya bila kufungana na Uturuki.
Kaka ni muumini mzuri wa Kikristo, anayeabudu madhehebu ya Evangelical Christian, tangu akiwa na umri wa miaka 12.
Mwaka 2002, katika fainali za Kombe la Dunia, Kaka aliwahi kuvua jezi yake na kubaki na fulana iliyokuwa na maandishi yaliyokuwa na ujumbe wa kumtukuza Mungu ‘God is faithful’.
Mbali ya soka, Kaka ni mpenzi mkubwa wa muziki wa Injili na mara nyingi husoma Biblia katika kujifunza neno la Mungu. Kwa maneno mengine, Kaka ni mlokole.
Hivi sasa mchezaji huyo anachezea klabu ya Ac Milan ya nchini Italia chini ya kocha Carlo Ancelotti, pia yupo kwenye kikosi cha timu yake ya taifa ya Brazili ambaco kinawania kufuzu kucheza la dunia ambalo kwa mara ya kwanza katika historia ya soka duniani linafanyika barani Afrika kule Afrika Kusini.
Huyo ndie Ricardo Izecson dos Santos Leite maarufu kama Kaka, mchezaji mwenye mafanikio zaidi ambaye anajivunia kumpenda mungu kutokana na wokuvo alioupata tangu akiwa na umri wa miaka 12.
Simu: 0719000010
E-mail:
jmihiko@yahoo.com