BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX
Photobucket

Thursday, May 19, 2011

KWA NINI MASHINDANO YA UREMBO TANGA YANAPOTEZA MVUTO..!!??

(Miss Tanga 2010 Anna Kiwambo, nafasi ya pili ni Jally Murei, wa tatu ni Zuleha Mrisho)

Hivi karibuni mashindo ya kumsaka mnyange wa Miss Tanzania 2011 yalizinduliwa rasmi katika hoteli ya kimataifa ya Kilimanjaro Kempnsiky. Haya ni moja kati ya mashindano maarufu sana hapa nchini ambayo huanzia katika ngazi za vitongoji, mikoa hadi kanda.

Chini ya uratibu wa kampuni ya Lino Agency na udhamini mnono wa kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom, mashindano haya yamekuwa yakipata msisimko na kuzidi kuwa maarufu hapa nchini.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni ya Lino International Agency Limited Bwana Hashim Lundenga, moja ya madhumuni ya mashindano hayo ni kuwakutanisha wasichana kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania , kujuana, kujenga urafiki na kujifunza mambo mbalimbali kutoka sehemu walizotoka. Zaidi pia kuitangaza nchi kimataifa.

Tangu mashindano haya yaliporejea mwaka 1994, kumekuwa na mafanikio mbalimbali, ikiwemo kukua kwa fani ya urembo, kuongezeka kwa ushiriki wa wasichana, kuongezeka kwa uelewa wa wananchi juu ya mashindano hayo pamoja na kutoa ajira kwa warembo mbalimbali.

Katika anga za kimataifa pia kumekuwa na mafanikio ya ushiriki wa kila mwaka katika mashindano ya mkumsaka mrembo wa dunia, kutangaza utalii na vivutio vya Tanzania , lakini pia mafanikio ya kushika nafasi nzuri katika mashindano ya dunia.

Mnyange Hoyce Temu, aliingia katika kumi bora mwaka 1999, huku Nancy Abraham Sumari akishinda taji la mrembo wa dunia kanda ya Afrika mwaka 2005, wakati alipoingia kwenye hatua ya fainali ya mashindano ya dunia na kushika nafasi ya tano katika mashindano ya mwaka huo. Hata hivyo historia hiyo haijavunjwa mpaka leo, ambapo mrembo wa mwaka 2010 Genevieve Emmanuel ndie anayeshikilia taji hilo kwa sasa na atamaliza muda wake hivi karibuni.


(Miss Tanga 2009 Glory Chuwa akiwa katika pozz pamoja na Rechal Mlaki namba mbili na Yasmini Zachari namba tatu.)


Wakati mashindao haya yakiendelea kupata umaarufu mkubwa hapa nchini kwa kuwa na msisimko na ushindani kuanzia katika ngazi za vitongoji, mkoani Tanga mambo yamekuwa yakibadilika ambapo mashindano hayo yanaanza kupoteza mvuto na hadhi yake.

Ili kupatikana mrembo wa Tanga atakayeuwakilisha mkoa kwenye mashindano ya Taifa au kanda mchakato huanzia kwenye vitongoji kama ilivyo kawaida katika sehemu zingine.

Vitongoji ambavyo vipo na tayari vimewahi kupeleka warembo kunako kambi ya Miss Tanga ni vya wilaya za Lushoto, Handeni, Pangani na Korogwe ambayo imeanza mwaka huu.

Kwa upande wa Tanga mjini vitongoji nguli ambavyo vimekuwa vikitoa warembo kupeleka kambi ya Miss Tanga ni Chumbageni, Ngamiani, Usagara, College pamoja na kitongoji cha Kati, yaani Tanga City Central.

Wakati ikionekana kwamba utamaduni wa watu wa Tanga unazorotesha mashindano hayo, kiasi cha kuyafanya kukosa msisimko katika miaka ya awali, kampuni ya Five Brothers Entertainment iliyokuwa ikiratibu mashindano ya vitongoji ilipewa jukumu la kuratibu mashindano ya urembo ya mkoa wa Tanga mwaka 2007 ambapo ilifanya mapinduzi mkubwa katika mashindano hayo mkoani hapa.

Kampuni hiyo ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mkurugenzi wake bwana Nassoro Makau ilifanikiwa kurejesha heshima na msisimko katika mashindano hayo mkoani hapa, ambapo moja ya mafanikio ya haraka ni kuweza kutoa mrembo aliyeshika nafasi za juu katika mashindano ya taifa. Naye ni Victoria Martin, aliyekuwa Miss Tanga. alishika nafasi ya nne katika mashindano ya Miss Tanzania 2007.

Licha ya hivyo, pia Victoria alichaguliwa kuwa Balozi wa kinywaji cha Redds yaani Miss Redds, na baadaye kushika nafasi ya tatu katika mashindano ya mrembo wa Afrika Mashariki mwaka 2009. Kwa sasa mwanadada huyu ni mwanamitindo.

Kabla ya Five Brothers mwaka 2007, kulikuwa na kampuni nyengine pia ziliwahi kuandaa mashindano ya Miss Tanga. Moja ya kampuni hizo ni Boy George Entertanment. Hii iliweza kutoa mwanga wa kutosha na kufanya watu wa Tanga wathamini mashindano haya.

Tangu alipofanya vizuri Victoria hadi sasa mkoa wa Tanga umekuwa ukihangaika kuifikia historia hiyo au kuivunja rekodi ya kutoa mnyange wa Tanzania miaka ya nyuma zaidi ya mwaka 2007. Lakini mkoa wa Tanga haukufurukuta sana . Lakini pia baada ya Victoria mkoa huu umeendelea kususua kwenye fani hiyo.


(Jally Murei ni Miss Tanga namba mbili aliyeuwakilisha mkoa mwaka 2010)

Pengine kumekuwa na tatizo ambalo ama linachangiwa na uratibu au kwa namna warembo wanavyochaguliwa. Kwa mfano mwaka 2009 na 2010 warembo waliochaguliwa na majaji walioitwa “mahiri”, hawakufanya vizuri kabisa kwenye mashindano ya kanda na hata taifa.

Miss Tanga 2010 Anna Kiwambo aliyechaguliwa na majaji
wenye ubora, hakuweza kufurukuta kwenye mashindano ya Kanda Kaskazini, na badala yake mshindi namba mbili kutoka Tanga Jally Murrei aliitoa Tanga kimasomaso kwa kushika nafasi ya tatu kwenye mashindano hayo na kwenda kuiwakilisha Tanga kwenye mashindano ya Miss Tanzania ni moja ya mambo yanayozua utata juu ya namna ya uchaguaji warembo.

Bada ya malamiko na mambo mengine kutoka kwa wadau mwaka huu mashindano hayo ya Miss Tanga yanaratibiwa na kampuni ya New Face Entertainment ambayo awali ilikuwa ikiandaa mashindano ya kitongoji cha Miss College . Haijulikanani ni kwa nini kampuni ya Five Brothers Entertainment imeachia ngazi. Hakukuwa na taarifa rasmi iliyotolewa zaidi ya minong’ono ya hapa na pale.

Ushauri wangu ni kuwa hali hii inaleta ukakasi kidogo, kwani pamoja na mashindano hayo kuonekana kupwaya kwa kiasi kikubwa jijini hapa, lakini pia waandaji wamesahau kuwa wanapotumia jina la MISS TANGA ni Tanga ile ile yenye wilaya 8, tarafa 37, kata 136 na vijiji 557. Hivyo isionekane ni mashindano ya mtu binafsi ama vinginevyo.

Pengine maslahi ni jambo ambalo linawekwa mbele sana kwa waandaji wa mashindano haya, na pengine maslahi hayo hayo ndio yanafanya Tanga iwe inatoa warembo wasio na sifa kila mwaka. Sio kweli kwamba Tanga haiwezi kutoa Miss Tanzania , siamini hilo ! Kama iliweza pia kutwaa nafasi ya tatu mwaka 1996 kupitia mrembo Mona Koja, kwanini basi leo isiweze kupiga hatua zaidi?

Imani yangu ni kuwa sifa za mabinti wa Tanga bado zipo pale pale, ukarimu wao, lugha yao laini, ufundi wao katika mapishi na hata urembo pia. Tanga ina sifa nzuri sana midomoni mwa Watanzania wengi, lakini wengi wamekuwa wakijiuliza swali kama nililojiuliza mimi. Kwanini Tanga haijawaji kutoa Miss Tanzania .

Kwa mfano, katika mashindano ya kitongoji cha Tanga City Central yaliyofanyika hivi karibuni yaliyoandaliwa na kampuni ya Green Apple Entertainment ni ushahidi tosha kuwa mashindano haya ya urembo yamepoteza mvuto mkubwa hapa Tanga kwa idadi ndogo ya watu waliohudhuria siku hiyo. Ilikuwa aibu ya mwaka. Hapo kabla kitongoji hicho hakikuwa hivyo. Naweza kusema ni moja ya kitongoji kinachofanya vizuri sana kwani ndicho kilichomtoa Rachel Mlaki 2009.

Majaji wa Miss Tanga 2009 walimpa nafasi ya pili kwenye mchakato huo. Cha kufurahisha mwaka uliofuata akiwa chuoni dodoma alitwaa taji la Miss Udom na kufanikiwa kuingia kambi ya Miss Tanzania . Huwa najiuliza, ni vigezo vipi wanavyotumia waandaji wa Miss Tanga katika kuwapata majaji bora wanaojua maswala ya urembo.

Lakini pia, swala kubwa lililopo hapa ni dhamana ya kampuni husika iliyopewa ili kuhakikisha mashindano hayo ya urembo yanautangaza mkoa wa Tanga kama moja ya madhumuni yaliyotajwa na waandaji wakuu wa mashindano haya nchini. Isionekane tu yapo kwa ajili ya kuitangaza nchi, bali pia yatumike kujitangaza kitaifa kwa maana ya mkoa kwa mkoa. Kwani leo anapopatikana Miss Tanga na kwenda kuuwakilisha mkoa wake, akawa Miss Tanzania sifa hivi ni za watu wa Tanga wote na sio kampuni iliyoandaa pekee.

Ombi langu kwa mkuu wa mkoa wa Tanga Meja Jenerali Msataafu Saidi Saidi Kalembo ni kuwa ayatazame kwa makini mashindano haya na waandaji wake pia. Isiwe anapewa mwaliko na kuhudhuria kama mgeni rasmi pasipo kujua utaratibu mzima wa uwandaaji wa mashindano yenyewe.

Labda majukumu ya kazi yatakuwa yanambana sana , lakini anaweza pia kutuma hata wajumbe ambao baadae watampelekea ripoti. Wayatazame haya kwa makini. Kwanza , uwezo wa kampuni inayoandaa mashindano ya Miss Tanga. Pili, kama kampuni hiyo imesajiliwa. Na tatu, kama ina kamati madhubuti inayotazama uzalendo kwanza, pamoja maslahi, ni muhimu pia.

Kwa kufanya hivi nadhani labda Tanga inaweza kutoa mnyange wa Miss Tanzania kwa mwaka huu wa 2011. Napenda kutoa shukrani kwa kampuni ya Five Brothers Entertainment kwani walifanya kazi nzuri ya kurudisha heshima ya mashindano haya. Pia kila la heri kampuni ya New Face Entertainment. Mchanga wa pwani huo!

Makala hii imeandikwa na..

Mohammed Hammie Rajab (Anko Mo)


No comments:

Post a Comment