BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX

Wednesday, April 13, 2011

MASIKA YAANZA KULETA MAAFA TANGA

MVUA za masika zilizoanza kunyesha kwenye maeneo tofauti nchini kuanzia katikati ya Machi, 2011, zimeanza kusababisha madhara kwa baadhi ya wakazi wa wilaya za Mkoa wa Tanga.

Mpaka sasa mvua hizo zimesababisha vifo vya wakazi wanane ambao saba ni kutoka wilaya za Handeni na Kilindi na mmoja jijini Tanga na uharibifu wa mali kutokana na miti mikubwa mikongwe kuanguka.

Akithibitisha vifo hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Jaffar Mohamed alimtaja marehemu Hamisi Hassan (45) mkazi wa Kata ya Makorora jijini Tanga ambaye alikufa juzi baada ya kuangukiwa na mti mkongwe kutokana na mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyokuwa ikinyesha hapa.

“Jumapili jioni majira ya saa 10 nilipata taarifa kwamba jirani na Soko la Uzunguni kuna mfanyabiashara wa kunoa visu (Hassan) ameangukiwa na mti mkubwa pamoja na magari kadhaa baada ya kusukumwa na upepo mkali wakati mvua ikiendelea kunyesha. Marehemu huyo alikuwa ameumia vibaya kichwani na alifariki muda mfupi akiwa Hospitali ya Bombo alikokuwa akipewa matibabu,” alisema Mohamed.

Akizungumzia matukio ya vifo vingine saba vilivyotokea wilayani Handeni na Kilindi, alisema vimetokana na watu hao kusombwa na maji ya mvua wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka mito iliyokuwa imefurika maji.

Alisema chanzo cha vifo hivyo ni wanavijiji kuamua kuweka mazoea ya kupita kwenye njia au maeneo ambayo yana mikondo ya mito ya muda mfupi pasipo kuhofia nguvu na kina cha maji yaliyopo.

“Unajua wakati mwingine mvua hizi za masika zimekuwa zikinyesha mfululizo mpaka siku hivyo wakati mwingine unakuta mwanakijiji amezoea kupita njia fulani ambayo ina mkondo wa mto hivyo bila ya kupata uhakika wa kina cha maji katika eneo kama hilo unakuta mtu anaamua kuvuka mto au mkondo huo wa maji kwa mazoea tu na hatimaye maji humshinda nguvu na kuzama,” alisema.

Amewatahadharisha wananchi kuacha mazoea ya kupenda kuvuka kwenye maeneo yasiyo rasmi hasa yenye mito ya maji pamoja na kukaa chini ya miti mikongwe wakati mvua zinapoendelea kunyesha.

Aidha, amewataka wazazi kuhakikisha wanaongeza uangalizi na usalama kwa watoto wao wadogo hasa wanaoenda shule kwa kuhakikisha wanarudi nyumbani kwa muda unaostahili wanapomaliza masomo ya siku ili kudhibiti uwezekano wa kuzurura ovyo, hivyo kukumbwa na ajali zinazoweza kusababishwa na mvua


Na Anna Makange, Tanga

No comments:

Post a Comment