BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX

Wednesday, June 16, 2010

'NAHISI NAOTA MPAKA SASA'- AT

Ikiwa ni siku chache tu zimesonga tangu msanii huyu ajinyakulie tuzo ya wimbo bora wa kolabo aliofanya na Stara Thomas wa 'Nipigie',msanii Ali Ramandani Ali 'AT'...anasema kutokana na mafanikio makubwa aliyoyapata kwa kipindi kifupi...hakika bado anajiona kama yupo ndotoni.

AT...anasema hajawahi kufikiria hata siku moja kama anaweza kuwachanganya wapenzi wa muziki kwa singo moja tu ya 'Nipigie' ambayo inaendelea kutamba katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni hapa nchini.

"Mafanikio ya singo hiyo yamenifanya niwe na kiburi, najiona ninaweza muziki pia ndoto zangu za kuwa mmoja wa watawala katika fani hii zipo mbioni kutimia."

"Napata shoo za kufa mtu mpaka nyingine nazikataa, yaani naringa najaa kiburi, kutokana na wimbo huo," anasema AT.

Mwanamuziki huyu mwenye asili ya Pemba lakini amejikita zaidi kwa wajanja 'Dar es Salaam', anasema hatua aliyofikia ni kubwa na kwamba anawatetemesha wakali wengine.

"Wakati nilipoanza muziki wengi hawakuamini kama ningefanya vema, sasa wengi wanakubali sikuwa nikifanya utani."

AT,ambaye anadai ametoka katika familia ya kimasikini anasema matunda ya wimbo huo yamemfanya atunze wazazi wake waliopo Zanzibar na vilevile anaishi vema pamoja na mchumba wake (hakutaka kumtaja jina)."Nimetoka kwenye familia ya kimasikini, hilo silikatai, nalikubali tena kwa moyo mmoja, napopata mafanikio anajiona mwenye amani zaidi."

..."Ingawa siwasaidii wazazi wangu katika kila kitu lakini nawapa kile kidogo ninachokipata kutokana na muziki hasa wimbo wa 'Nipigie'," anasema AT.

Anasema ingawa yeye ni mtu wa watu lakini wimbo huo umemfanya atembee mabega juu zaidi.

"Kuna maringo ya kujisikia na ya kujiamini, mimi nina maringo ya kujiamini ndiyo maana ni mtu wa watu napenda kukaa uswahilini kujichanganya na watu kwa sababu hao ndiyo wanaonifanya niwe juu,"anasema AT.

AT ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya tisa wa familia yao anasema hakuna kitu kizuri kama kujichanganya na wadau mitaani kwani hao ndiyo wanaofanya wasanii wawe juu siku zote kwa kununua CD zao na kuingia kwa wingi kwenye shoo zao.

Mwanamuziki huyo aliyezaliwa miaka 26 iliyopita katika Hospitali ya Mwembeladu, Zanzibar anasema mwanamuziki hatakiwi kudharau watu mitaani kwa sababu ya kuwa nyota.

AT pia anaamini amepata Tuzo ya Muziki ya Kili kutokana na ushirikiano alioupata kutoka kwa watu wa mitaani.

Akieleziea wimbo huo anasema: "Wazo wa la kuimba 'Nipigie' lilinijia kama masihara na sikujua kama wimbo ungepanda chati kiasi cha kunipatia tuzo."

AT, anatarajia kuzindua albamu yake iliyobeba jina la 'Nipigie' yenye nyimbo 14 hivi karibuni. Albamu hiyo ina vionjo vya sauti za wanamuziki kama Nyota Ndogo, Nameless, Ngoni, Shircom, Stara Thomas,Tina, Hadija Kopa na Joti pia inamiondoko mbalimbali, kama ya Zuku, miondoko ya Afrika Magharibi na mchanganyiko wa lugha ya Kiswahili na Kiarabu.

"Wimbo huo umenifanya nikutane na watu wazito ambao sikutegemea kukutana nao katika maisha yangu ya muziki, namshukuru Stara Thomas kwa kushirikiana nami," anasema AT.

Na mwanamuziki huyo anasema anatarajia kuachia singo nyingine kali ambayo anaamini itakuwa na mafanikio makubwa.

Mbali na nipigie AT ameimba nyimbo kama Wanimaliza,Mapenzi,Raha Zako, Kwanini,Yamini,Vijana,Utaona Noma,Ziro na nyinginezo.

Baadhi ya nyimbo zake zimefanywa kwa maproducer wakali kibao kama kwa Benjamin wa Mambo jambo, Marco Chali na wengine kibao.

No comments:

Post a Comment