BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX
Photobucket

Wednesday, July 27, 2011

ALBINO KUPANDA MLIMA KILIMANJARO

KATIKA kukabiliana na dhana potofu iliyojengeka katika jamii dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwamba hawana uwezo sawa na wengine, Josephat Torner ameamua kuvunja ukimya kwa kupanda Mlima Kilimanjaro.

Anatarajia kuanza safari yake hiyo itakayomchukua siku nane, Jumamosi wiki hii kuelekea kileleni kwa lengo la kuithibitishia jamii ambayo bado inaendeleza vitendo vya ukatili na unyanyapaa dhidi ya albino kwamba wao wanaweza kufanya kila kitu.

Torner ametoa kauli hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari na kusema lengo pamoja na kufikisha ujumbe huo muhimu ni kuwa albino wa kwanza Tanzania kufanya kitendo hicho cha kishujaa cha kufika kwenye kilele cha Kilimanjaro, mlima mrefu barani Afrika.

“Nipo mbele yenu hapa leo kuweka msimamo dhidi ya mawazo potofu yaliyopo katika fikra za baadhi ya Watanzania na Waafrika wengi ambao wanaamini kwamba albino hana uwezo sawa na watu wengine, fikra hizi ni hatari zimeendelea kusababisha ubaguzi, kutengwa, ukatili na mauaji dhidi yetu kwa muda sasa,” amesema.

“Jumamosi ya Julai 30, mwaka huu, nitaanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro lengo kuu ni kufikisha haki za albino kileleni mwa Afrika na kutangaza kwa sauti kubwa niwezavyo kwamba albino sio mtu wa kuogopwa, kubaguliwa, anayestahili kuwindwa kama mnyama wa porini akikatwa vipande kwa ajili ya biashara, bali ni binadamu kama wengine.”

Torner amebainisha kuwa, uamuzi wake huo umetokana na kasi ya vitendo vya ukatili na mashambulizi yanayoendelezwa na baadhi ya Waafrika kutokana na imani za kishirikina zilizochochea biashara ya viungo vya albino na kusababisha madhara mengi kwao hasa kulazimishwa kuishi kwa wasiwasi.

“Nitakapopanda mlima nitapanda kwa ajili ya albino wote waliolazimishwa kuondoka nyumbani kwao kwenda kuishi kwenye kambi maalumu zinazowatenga na familia zao na kuwapa upweke na kuwaambia iwe mwisho wa kujificha kwenye kivuli cha jua tena, ndoto yangu ni kuunganisha albino wote ili tuuthibitishie ulimwengu tuna uwezo sawa na binadamu wengine ila tunatofautishwa na mahitaji,” amesema.

Takriban miaka mitano sasa, hali ya albino nchini imekuwa si shwari kutokana na kasi ya ushambuliaji, uwindaji na mauaji ya kikatili yaliyosababisha vifo zaidi ya 60, huku Serikali ikilazimika kuhamisha wanawake na watoto 118 katika shule maalumu ili kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha yao dhidi ya wawindaji.


Na Anna Makange, Tanga.

No comments:

Post a Comment