Kocha Mkuu wa timu ya soka mkoa wa Tanga chini ya miaka 17 iliyoshiriki mashindano ya Copa Coca Cola yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Raphael John amefungiwa kufundisha soka kwa kipindi cha mwaka mmoja. Uamuzi huo ulitolewa juzi na Makamu mwenyekiti wa TRFA mkoa wa Tanga,Mustafa Selleboss kwenye kikao cha kamati ya utendaji wa chama hicho kilichoketi katika ofisi za chama hicho jijini Tanga.
Selleboss alisema kuwa kufungiwa kwa kocha huyo kunatokana na kudaiwa kudanganya umri wa wachezaji walioshiriki ligi hiyo ambayo walidaiwa kuwa ni vijeba. Makamu mwenyekiti huyo alieleza kuwa adhabu ya kwanza kwa kocha huyo wa soka ni ya kufungiwa na shirikisho la soka hapa nchini (TFF) kwa miezi sita kwa kubainika kufanya udanganyifu huo.
Aidha adhabu ya pili aliyotolewa na chama cha soka mkoa wa Tanga (TRFA) ambapo amefungiwa miezi sita ambapo atatumikia adhabu ya pili baada ya ile ya kwanza kumalizika. Viongozi wengine waliopewa adhabu ni wale walioambatana na timu hiyo kwenye mshindano hayo ambapo Mohamed Kampira ambaye alikuwa kocha msaidizi,alisimamishwa kwa miezi mitatu kutojihusisha na soka.
Makamu mwenyekiti huyo wa TRFA pia alitoa wito kwa walimu wanaokabidhiwa timu wawe wakweli katika taratibu mbalimbali lengo likiwa kunusuru timu zinazoshiriki. Aidha kikao cha kamati ya utendaji wa TRFA kiliketi kujadili mwenendo mzima wa soka mkoani Tanga na ushiriki wa Coastal Union katika ligi daraja la kwanza ngazi ya taifa ikiwa ni mwisho wa kurejesha fomu kwa timu zitakazoshiriki.
Pia kikao hicho kilifanya kazi ya kupitia barua ya ongezeko la idadi ya timu zinazotarajiwa kushiriki ligi ya mkoa msimu wa 2010 hadi 2011.
No comments:
Post a Comment