MTU mmoja anayedhaniwa kuwa jambazi ameuwawa na wananchi wenye hasira kwa mapanga na mawe baada ya kushindwa jaribio la uporaji katika Taasisi ya fedha ya Brac iliyoko Mikanjuni jijini Tanga.
Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 6.30 mchana baada ya watu wane wanaodhaniwa kuwa majambazi kuvamia taasisi hiyo na kuwaweka chini ya ulinzi wafanyakazi wa Taasisi hiyo huku wakiwa na silaha aina aina ya Shotgun iliyokatwa mtutu na kufanikiwa kupora kiasi cha shilingi Milioni 12.
Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Tanga RCO Jaffar Mohamed akizungumza na waandishi wa habari alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza baada ya Mlinzi wa Taasisi hiyo Bw.Juma Mussa alipiga kelele na watu kutoka sehemu mbalimbali na kulizingira eneo hilo na kufanikiwa kuwazidi nguvu majambazi hao kwa mapanga na mawe ambapo mmoja wa jambazi hilo akalazimika kutupa begi la fedha alizoiba.
RCO Mohamed alisema baada ya purukushani hizo Polisi waliwahi kufika eneo hilo na kuwadhibiti majambazi ambapo Polisi ilimchukua jambazi huyo Iddy Ramadhani(30) Mkazi wa Mwanzange jijini Tanga kumpeleka hospitali ambapo alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo.
Alisema jambazi huyo amekuwa na rekodi ya tuhuma mbalimbali za uhalifu hasa umiliki wa silaha ambapo wenzake walishawahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Hata hivyo Polisi walifanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi Milioni 9.7 zilizokuwa zimeporwa huku Mil.2.1 zikiwa zimepotea katika eneo hilo .
Polisi wanaendesha msako kuwatafuta majambazi wengine waliotoroka katika tukio hilo huku Jeshi hilo likitoa wito kwa Taasisi za Fedha kutoweka fedha nyingi katika ofisi zake kama hakuna ulinzi. Pia Jeshi hilo lilipongeza juhudi za wananchi wa eneo hilo kwa kutoa taarifa mapema na kufanikiwa kuokoa kiasi hicho cha pesa.
Hili ni tukio la kwanza la ujambazi kutokea Mkoani Tanga tangu kuondoka kwa aliyekuwa Kamanda wa Polisi Simon Sirro ambaye kwa sasa amehamishiwa Mkoani Mwanza.
No comments:
Post a Comment