WAENDESHA pikipiki za bodaboda wapatao zaidi ya 50 wameandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mathew Nasei wakidai mwenzao amepigwa na askari polisi na kuwekwa mahabusu.
Tukio hilo la kuandamana vijana hao lilitokea juzi majira ya saa 3:00 asubuhi wakiwa na pikipiki zao huku wakiwa wanapiga honi na kuimba.
Vijana hao baada ya kufika katika ofisi za mkuu wa wilaya walimuona na kumueleza kwamba kuna mwenzao amepigwa na polisi na kuwekwa mahabusu kwa madai amekaidi amri ya polisi.
Mmoja ya vijana hao wa bodaboda , Selemani Juma akizungumza na mkuu wa wilaya kwa niaba ya wenzake, alisema polisi walifika maeneo ya kituo cha mafuta cha BP na kumkuta dereva wa pikipiki ya bodaboda amekaa juu ya pikipiki yake huku ikiwa imeiegesha.
Alisema polisi hao walimhoji kijana huyo aliyekuwa amekaa katika pikipiki yake kuwa aonyeshe leseni yake na kofia ya pikipiki.
Juma alisema kuwa kijana huyo aliwajibu polisi kwamba hana kofia aliiacha kwa sababu haendeshi pikipiki bali alikaa juu ya pikipiki hiyo.
Alisema baada ya kijana huyo aliyekuwa amekaa katika pikipiki hiyo kujibu hivyo, polisi walianza kumpiga wakidai aliwaletea jeuri wakiwa kazini na kumpeleka mahabusu katika kituo cha polisi.
Hata hivyo akijibu malalamiko hayo mkuu wa wilaya alisema kuwa tatizo lao atalishughulikia baada ya kuzungumza na upande wa pili yaani polisi, lakini hawezi kusikiliza upande mmoja.
Alisema kuwa yeye anajukumu kubwa la kutetea wananchi, lakini akasema kuwa waendesha pikipiki za bodaboda wamekuwa na tabia ya kuvunja sheria ya kukaidi kuvaa kofia pamoja na kwenda mwendo wa kasi.
Na Steven William, Muheza
No comments:
Post a Comment