BLOG HII IMEDHAMINIWA NA: MWEKASU HOSTEL, PWEZA NIGHT CLUB TANGA, SOPHIA PRODUCTION, AFRICAN DESIGN, BREEZE FM, PANGANI COAST CULTURAL TOURISIM PROGRAMME, NA SAFARI LODGE ANNEX

Friday, September 17, 2010

MIFARAKANO YA WANANDOA CHANZO CHA WATOTO YATIMA MUHEZA!!

MIFARAKANO kwa baadhi ya wanandoa kwenye jamii,imetajwa kuchangia tatizo la kuzagaa kwa watoto wa mitaani katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Muheza Mkoani Tanga. Katibu Msaidizi wa Kituo cha kulelea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu cha Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu cha Kharia kilichopo mjini Muheza Mkoani Tanga, Bibi Hidaya Kilua amesema hayo wakati akizungumza na Blog hii juu ya tatizo la watoto wa mitaani wilayani humo.

Bibi Hidaya amesema kufarakana kwa baadhi ya wanandoa, kufariki dunia kwa wazazi kutokana na ugonjwa wa UKIMWI ni moja ya sababu zinazochangia kuendelea kuwepo kwa watoto yatima na wale waishio katika mazingira magumu wilayani Muheza. Amesema jamii Mkoani Tanga haina budi kuepukana na migogoro katika familia ili kupunguza tatizo hilo la watoto yatima na waishio kwenye mazingira magumu.

Amesema kwa sasa kituo hicho kinajumla ya watoto yatima 40 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Muheza ambao wametelekezwa kutokana na wazazi wao kutengana huku wengine wakiwa wamefariki dunia ambapo kwa sasa kituo hicho kimechukua jukumu la kuwalea na kuwasomesha kwa maendeleo yao ya sasa na baadae.

Ameiomba Serikali kuelekeza nguvu zake kusaidia vituo vya kulelea watoto yatima ili waweze kupata haki zao kama watoto wenye wazazi wao ikiwemo matibabu mazuri,elimu,mavazi na makazi bora.

Na Benedict Kaguo, Muheza

No comments:

Post a Comment