WANAWAKE wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga wamtaka mke wa Rais Jakaya Kikwete kuwaombea kwa kiongozi huyo wa nchi ili waweze kugaiwa mashamba ya mkonge yasiofanya kazi lengo likiwa kuwawezesha kuendesha kilimo kwa tija.
Wanawake hao walitoa maombi yao hayo kupitia risala yao iliyosomwa na katibu wa CCM wilayani Muheza Josephen Mbezi ambapo alisema kuwa iwapo kanda hiyo itapatiwa mashamba hayo wanawake wataweza kujishughulisha na kilimo kwa ufanisi.
Mbezi alisema ni vyema kwa mashamba hayo kugaiwa kwa wananchi hususani wanawake wa wilaya hiyo ya Muheza lengo likiwa kuwawezesha kujishughulisha ambapo wataweza kujisaidia ikiwani pamoja na kuinua pato la familia zao.
Kwa upande mwingine katibu huyo wa CCM wilayani Muheza alimweleza mke wa Rais mama Salma Kikwete kwamba wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa hospitali ya wilaya ambapo sasa wamekuwa wakipata huduma kupitia hospitali ya taasisi ya kidini.
Akijibu suala la ukosefu wa hospitali ya wilaya mama Salma aliwataka wananchi hao kuondoa hofu kwamba hawana hospitali hiyo kwenye eneo lao na kuwaeleza kuwa serikali inachangia robo tatu ya gharama za uendeshaji ila mpango upo wa kujijenga.
“Pale muende kifua mbele serikali yenu inajitahidi kuwasaidia wenye jingo hilo ambao ni taasisi ya dini kwa tatu ya nne ambapo ni mishahara,madawa na vitendsea kazi,lakini hata hivyo mpango upo wa kujenga hospitali yenu ya wilaya”alisema mama Kikwete.
Akizungumzia zaidi masuala ya afya mama Salma alisema, serikali ya CCM imeweza kujitahidi kujenga zahanati ili kuhakikisha kwamba angalau watu hawatembei zaidi ya kilomita tano kwa ajili ya kufuata huduma za afya kwenye maeneo wanayoishi.
Kwa upande wa sekta ya elimu mama Kikwete,alisema mpango madhubuti unaendelea kufanya kazi ya kupika walimu katika chuo kikuu cha Dodoma ambapo hata hivyo suala la ujenzi wa maabara na kuweka vitendea kazi tayari bajeti yake imeandaliwa.
Amewahimiza wanawake kusoma pamoja na kuwasomesha watoto wao pia kuepuka kuwaozesha ovyo jambo ambalo limekuwa likichangia kuzorotesha maendeleo yao huku akisisitiza kuwepo kwa mpango wa uwezeshaji kwa wanawake ili kuinua uchumi wao.
Aidha mama Kikwete alisisitiza umuhimu wa wanawake kuthubutu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi huku akihimiza mshikamano miongoni mwao ili kutoa fursa kwao kushika madaraka katika nchi hii ili kuweza kufikia lengo la hamsini kwa hamsini.
Vilevile mke huyo wa Rais ambaye ni Mwenyekiti wa WAMA,mama Kikwete aliwataka wanawake kuona umuhimu wa kuchagua viongozi wa CCM ili kupata maendeleo zaidi katika nchi yao ambayo bado chama tawala kinahitaji ridhaa yao.
“Hapa Muheza nazi si ziko nyingi? basi mama unapokuna nazi ukipeleka kushoto unataja Diwani..diwani,ukipeleka kulia,mbunge..mbunge na ukifika katikati ndio unamaliza tena unasema Kikwete..kikwete hapo ndio utapata mafiga matatu”alisema mama Salma.
No comments:
Post a Comment